Miradi ya ufugaji miongoni mwa jamii ya vijana katika maeneo mengi nchini imechangia pakubwa ukuaji wa uchumi wa taifa hili.
Katika siku za hivi majuzi vijana katika Kaunti ya Kisumu walikuja pamoja na kuunda vikundi kwa madhumuni ya kujiendeleza kupitia miradi mbalimbali.
Katika Kaunti Ndogo ya Kisumu Magharibi, vijana wametia fora kwenye maendeleo, hali ambayo imebadilisha pakubwa maisha yao na kupanua ajira miongoni mwa jamii za eneo hilo.
Katika maeneo ya Kolenyo, Kombewa, Mamboleo na Kisian vijana wameimarisha maisha yao baada ya kuanzisha miradi mbalimbali inayowapa ujira dhabiti wakiwa pamoja katika vikundi.
Kikundi cha Faida Youth Group kilichoko katika Wadi ya Kombewa kimestawi baada ya kunufaika kutokana na mradi wa ufugaji wa kuku ambao umedumu kwa miaka miwili iliopita.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Remjeus Okoth aliyeongea na Mwandishi huyu wa habari siku ya Jumamosi alisema mradi huo unanuia kuwapa faida ya kiasi cha hadi nusu milioni ifikapo mwakani.
''Ifikapo mwishoni wa mwaka huu tutakuwa tunakadiria faida ya zaidi ya nusu milioni ambayo itatokana na mauzo ya kuku wa nyama na mayai,'' alisema Okoth.
Aidha, mwenyekiti huyo alidokeza kuwa kikundi chao kimegawanywa katika vikundi vitatu ambavyo vimepewa utunzi wa kuku chini ya uangalizi wa viongozi walioteuliwa.