Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amewaonya vikali vijana wanaotumiwa na baadhi ya watu flani kuwafurusha wakazi na kunyakua ardhi zao pamoja na zile za kibinfsi kukoma mara moja la sivyo watakabiliwa kisheria.

Kulingana na Marwa, kuna baadhi ya vijana wanaopewa pesa na mabwenyenywe wanaoshirikiana na baadhi ya maafisa tawala kuwafurusha wakazi katika ardhi zao pamoja na kunyakua ardhi za watu binafsi akisema kwamba watakabiliwa na maafisa wa usalama.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Marwa alisema kwamba hatua hiyo imechangia kuwepo kwa migogoro ya ardhi na kukithiri kwa visa vya uhalifu katika kaunti hiyo, hali ambayo huenda ikaleta migawanyiko baina ya jamii.

“Tunawaomba vijana kujitenga na baadhi ya watu flani wanaowapa pesa na kuzua vurugu na kunyakua ardhi za wakazi pamoja na zile za kibinafsi, hilo hatutakubaliana nalo na lazima sheria kali zichukuliwe dhidi ya watu kama hao,” alisema Marwa.

Aidha, amewataka wakazi kuwaripoti vijana hao kwa maafisa wa usalama ili kutiwa nguvuni na kuwasaidia maafisa wa usalama kutambuwa mabwenyenye wanaowatumia vijana hao vibaya na kukabiliwa kisheria ili kusitisha mogogoro hiyo.

“Tunawahimiza wakazi kuwapa habari maafisa wa polisi kuhusu vijana kama hao ili watiwe nguvuni na kuzuia kuwahangaisha wakazi katika ardhi zao,” aliongeza Marwa.

Kamishna Marwa ameahidi kutuma maafisa wa usalama mashinani kuwasaka vijana hao pamoja na mabwenyenye wanaotekeleza uhalifu huo ili kukomesha kuhangaishwa kwa wakazi katika ardhi zao na zile za kibinfsi katika kaunti hiyo ya Mombasa.