Mbunge wa Bomachoge Chache Simon Ogari amewataka Vijana wa kundesha piki piki kujiepusha na uhalifu, na badala yake kujiunga na makundi ambayo yatawafaa kiuchumi na kukua kimaisha.
Ombi hilo lilitolewa baada ya vijana hao kuhusishwa na visa vya uhalifu katika mji wa Ogembo na viunga vyake, ambapo hushirikiana na vijana wengine kuwaibia wateja.
Mbunge huyo ambaye alikuwa katika ziara ya kuwakabidhi pesa za miradi siku ya Jumanne katika mji wa Ogembo aliwashauri vijana wote kwa jumla kujihusisha na masuala ya maendeleo kwa kutumia hela wanazopata kutoka taasisi mbalimbali za kifedha na zile za Uwezo Fund kuwekeza kwenye miradi kama ufugaji na biashara nyinginezo.
“Kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi ambayo itawafaidi kwenye shughuli zozote kama kilimo cha mimea na ufugaji na kuweza kurudisha kiwango cha hela mnakopa kupitia Uwezo Fund,” alishauri mbunge huyo.
Baadhi ya vijana ambao walihudhuria hafla hiyo ya kupokezwa hela za Uwezo Fund wamshukuru mbunge huyo na kuahidi kuwa watawashauri vijana wengine kuacha kujihusisha na makundi ya vijana ambao huwapotosha na kuwaingiza katika uhalifu.
Mbunge huyo aliwashauri wakazi wote waache kuogopa kukopa pesa kutoka taasisi za kifedha, huku akiwaambia kuwa sharti wawe wa uwajibikaji mkubwa wanapoomba mikopo kama hiyo ili kujiepusha na migogoro na mashirika husika.
Zaidi ya shilingi milioni nane zilikabidhiwa makundi mbali mbali ya vijana na kina mama wa eneo bunge hilo.