Vijana katika Kaunti ya Kisumu wametakiwa kutumia taaluma yao kujiendeleza ili kushiriki vikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Mwakilishi wa Kaunti Ndogo ya Seme, George Gwanda, aliwataka vijana katika eneo hilo kujianzishia kazi kutokana na taaluma zao ili kumaliza umasikini miongoni mwa jamii na kuchangia kuinua uchumi wa Kaunti ya Kisumu.
Gwanda aliwaambia vijana kupitia ujumbe rasmi wa ripoti ya maendeleo ya vijana kutoka ofisi yake, mnamo siku ya Alhamisi kwamba nafasi za kazi zimefunguliwa kwa vijana na kuna haja kwao kuonyesha nia ya kujiendeleza kwa kuwajibikia vikamilifu.
''Wakati umewadia kwa vijana kuamka na kuchangia vikamilifu katika maendeleo ya nchi kwa kufanya kazi kutokana na taaluma yao,'' alisema mkuu huyo.
Alikariri kiongozi huyo kuwa vijana wengi katika eneo hilo wamesomea taaluma mbalimbali, na hivyo basi hawanabudi kutumia taaluma hizo kujiendeleza.
Katika Kaunti ya Kisumu vijana wametia fora kwenye maendeleo mbalimbali wakati ambapo wanashiriki katika miradi kadhaa ya kijuakali.
Juzi serikali kuu na zile za Kaunti nchini zilishirikiana kuwapa vijana nafasi za kazi kwa kuwapiga jeki kwenye miradi yao kupitia mradi wa hazina ya maendeleo ya vijana ya, Uwezo Fund.