Wakazi wa eneo la Orije vitongojini mwa mji wa Kisumu wamelalamikia vikali wizi wa baisikeli ambao unaendelea kukita mizizi miongoni mwa vijana wa eneo ilo.
Wakazi hao walimlalamikia mkuu wa ulinzi wa mtaa katika eneo hilo, maarufu kama Nyumbani Kumi, Meshark Masanga na kusema kuwa vijana wa eneo hilo wamekosa kujishughulisha katika kazi za kukimu mahitaji yao na badala yake wameingilia wizi.
Wakizungumza katika mkutano wa usalama wa kijiji ulioandaliwa na mkuu huyo siku ya Jumapili, wakazi hao walitaka vyombo husika kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria vijana wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya wizi.
''Wizi ni baadhi ya mambo yanayochangia utovu wa usalama na kusababisha ukosefu wa maendeleo katika jamii,'' alisema Tom Wiswa, mwanachama wa kikundi hicho.
Wakazi hao pia waliwalaumu fundi wa baisikeli wa eneo hilo ambao wamesemekana huwasaidia vijana hao kubadilisha vifaa kutoka kwa baisikeli zilizoibiwa ili kusaidia kuficha ushahidi.
Walitishia kuwashitaki fundi wa baisikeli watakaopatikana wakijihusisha na vitendo vya aina hiyo.
Wiswa aliwaonya vijana wanaoshukiwa kuwa wezi kukoma tabia hiyo mara moja ama wakabiliwe na mkono wa sheria.
Aidha alisema ni idadi ndogo ya vijana wanaofanya mambo hayo, ikizingatiwa kuwa jamii ya vijana wamebuni makundi ya kimaendeleo na hawana wakati wa kuingilia tabia hiyo potovu.