Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vijana wametakiwa kutumia pesa za hazina ya maendeleo ya vijana na Uwezo Fund vizuri ili kuafikia maendeleo thabiti maishani.

Haya ni kwa mujibu wa kiongozi wa kamati ya urasibu wa hazina hiyo katika Wadi ya Siany iliyoko katika Kaunti Ndogo ya Kisumu Kaskazini, Boniface Odhiambo.

Akizungumza siku ya Jumatatu alipokutana na kikundi cha vijana kijulikanacho kama, Konyri Kendi ambacho kinajiendeleza na mradi wa kufuga samaki, Kiongozi huyo aliwataka vijana katika eneo hilo kushiriki vikamilifu katika ujenzi wa taifa kwa kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kujinufaisha na hazina hiyo ya serikali.

“Serikali kuu na ya Kaunti kwa pamoja zimejitolea kustawisha maendeleo nchini kupitia makundi ya vijana ili kuafikia maendeleo dhabiti na pia kutimiza ruwaza ya 2030,” alisema Odhiambo.

Odhiambo alisema kuwa tangu serikali ilipoanza kudhamini vijana katika vikundi, vijana wengi nchini wameshuhudia maendeleo miongoni mwao, ambapo kufikia sasa, wengi wanao uwezo wa kujitegemea maishani.

Aliongezea kuwa mbali na makundi ya vijana kufaidi pakubwa jamii, serikali zote mbili zimeweza kushuhudia ukuwaji wa uchumi nchini.