Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amewataka vijana kutoka kaunti hiyo kutumia talanta zao kujipatia kazi badala ya kutumiwa vibaya na wanasiasa na kupoteza mwelekeo kwenye maisha ya baadaye.
Akiwahutubia zaidi ya vijana elfu moja waliokongamana katika ukumbi wa umma wa Cultural mjini Kisii katika kusherehekea siku kuu ya vijana duniani siku ya Jumatano, Ongwae alisihi vijana ambao wana talanta mbali mbali kutilia maanani vipaji vyao kwa vile talanta ina pesa mno kuliko kazi za ofisi.
Gavana pia alidokeza kuwa kaunti ya Kisii iko katika mstari wa mbele kuinua vipaji kupitia wizara ya utamaduni na michezo, na kuwashauri kujiandikisha na idara husika ya vipaji ili kuweza kutambulika.
Aliwataka vijana waliohudhuria hafla hiyo kuacha kutumiwa vibaya na wanasiasa kama vile kuleta fujo kupitia maandamano, ambapo aliwataka kufuata utaratibu wa kisheria wanapowasilisha malalamishi yao kwenye ofisi za kaunti ili kutafutiwa suluhu.
Kongamano hilo ya kuadhimisha siku kuu ya vijana duniani lilianza siku ya Jumatatu na kukamilika tarehe 12, ambayo ndio siku halisi ya vijana ambayo husherehekewa kila mwaka.
Pia gavana alisema kuwa wataweka mipango maalumu ili kuona vituo vya kuwafaidi vijana kuendeleza talanta yao vinajengwa, na kuwashauri kuendelea kuimarisha michezo kama vile soka na riadha kwa kutumia vizuri uwepo wa nyuga za taasisi mbali mbali na zile za shule ili kukomaa kimichezo.