Ukosefu wa mtaji umetajwa kuwa chanzo cha vijana wengi kukosa kuanzisha miradi ya kuwainua kimaisha na kusababisha baadhi yao kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe haramu.
Akiongea siku ya Jumatano katika ukumbi wa umma wa Cultural Centre mjini Kisii, kiongozi wa vijana ambaye pia ni mjasiriamali wa masuala ya kilimobiashara, Bwana James Makori alisema kuwa hali hiyo huwanya wengi kupoteza matumaini kabisa ya kuishi.
Hata hivyo, aliwaomba vijana kujiunga kwa makundi ili kuboresha na kuimarisha akiba yao ya mapato na kuacha kutegemea kupata kazi za ofisi ili waanze miradi ya kuwakimu kibiashara na kilimo.
Aliwataka vijana kuwa na mtindo wa kuweka hela kidogo kidogo ili kuanzishia miradi.
Makori ambaye pia hujihusisha katika ushauri na nasaha kwa vijana jinsi ya kutumia na kuwekeza hela kwenye miradi, hasa inayohusiana na ukulima, aliwasihi vijana kuwa na umoja na kutembelea viongozi wao ili kupata mikopo ya fedha za ustawi wa maendelea maeneo bunge.
"Taasisi za fedha, kama vile benki pamoja na mashirika ya vyama vya ushirika, vinapaswa kuanza kuwa na imani kwa vijana. Mashirika haya yanastahili kuwapa mikopo ya kundeleza miradi yao ili kuwafaa vijana hao na kuwaepusha na shughuli za uhalifu ambazo mara nyingi husababisha wengi kuuliwa kwa risasi au kuchomwa na wakazi,” alisema Makori.