Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Kitutu Chache Kusini amesema kuwa vijana zaidi watasajiliwa katika Idara ya NYS tarehe Septemba 28 na kuwataka vijana kujitokeza siku hiyo ili kuandikishwa rasmi kwenye kikosi hicho.

Akiongea katika eneo la Nyanchwa siku ya Jumatatu, kwenye hafla ya kuwaruhusu vijana hao kuenda katika likizo ya wiki mbili, Mbunge Momoima Onyonka alisema kuwa analenga wale vijana ambao walikosa kupata nafasi katika usajili wa awali na kuwataka vijana hao kuendelea kujihusisha na shughuli zingine za kuboresha mitaa wanayotoka.

Onyonka pia aliwataka vijana wengine kutoka eneo bunge lake kujiepusha na masuala ya uhalifu kwa kisingizio kuwa hawana kazi.

“Wale ambao hawatafanikiwa kujiunga na NYS watafuea mbinu nyingine ya kujiinua kiuchumi kwani uhalifu hauna riziki,” alisema Onyonka.

Mbunge huyo aliahidi atahakikisha kuwa vijana wote pamoja na wakazi wote wanahusishwa katika shughuli zaa kimaendeleo na akawataka kuunda makundi na vyama vya kuomba mikopo ili wafanye miradi muhimu kama biashara na ukulima.

Alisema kuwa idadi ambayo walisajili hapo awali ya 1,400 huenda ikarudufishwa ili kuwapa vijana wengi nafasi kwenye kikosi hicho.

Onyonka aliwashukuru vijana ambao wameonyesha ukakamavu na juhudi kuu za kuboresha maneo mbali mbali katika mji wa Kisii kama vile kufanya usafi kwenye masoko pamoja na vituo vya magari na kuwataka kuendelea hivyo.