Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira, Timothy Bosire, ameomba viongonzi na wanasiasa wote kutoingiza siasa kwa maendeleo na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika sherehe ya mazishi ya mzee Joseph Atuya katika eneo la Tombe, mbunge huyo aliomba viongozi kufanya maendeleo na kuweka masuala ya kisiasa kando.
“Siasa katika maendeleo ndizo zimerudisha maendeleo nyuma. Naomba viongozi tufanye maendeo ili tutimize ahadi tulizowaahidi wananchi wetu wakati wa kampeini. Ifikapo 2017 tutaanza siasa rasmi lakini kwa sasa tuachane na mambo hayo,”alisema Bosire.
Bosire pia aliwaaomba viongozi wa eneo hilo kuepukana na ufisadi unaoshuhudiwa nchini.
“Naomba wananchi tuweze kuombea nchi hii ili tumalize masuala ya ufisadi kuendelea kushuhudiwa nchini. Tukiwa pamoja nina imani kuwa kila jambo litapata suluhu halisi,”aliongeza Bosire.
Matamshi ya mbunge huyo yaliungwa mkono na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nyamira Alice Chae ambaye alikuwa kwa mazishi hayo na kusema uwazi unastahili kuonyeshwa katika serikali za ugatuzi na ile ya kitaifa ili mwananchi wa kawaida kunufaika kikamilifu.
“Baada ya miaka mitano najua kila mwananchi atahitaji kujua yale viongonzi wamefanya kabla ya kuwachagua viongonzi wengine. Ni heri viongozi wote wa serikali za ugatuzi na wale wa serikali ya kitaifa tuwe na uwazi kwa maendeleo,” alisema Chae.