Pendekezo la kinara wa Cord Raila Odinga kwamba bunge za kaunti zote nchini ziruhusiwe kuchangia mijadala yao kwa lugha za mama, limepingwa na baadhi ya viongozi wa Kaunti ya Nakuru.
Wakizungumza siku ya Jumamosi baada ya hafla ya maombi yaliyoandaliwa na tawi hilo, kumwombea Naibu wa Rais William Ruto na Mtangazaji Joshua arap Sang, katika bustani ya Nyayo Gardens mjini Nakuru, viongozi wa chama cha TNA tawi la Nakuru, wakiongozwa na mwenyekiti wao Dkt Abdul Noor, wamemtaka kiongozi huyo wa upinzani kuacha kupotosha taifa na pendekezo hilo.
“Taifa hili si la kabila moja. Haiwezekani bunge 47 ziongee kila moja kabila lao. Hapa Nakuru tutazungumza lugha ipi kwa sababu ni eneo lenye makabila yote. Ni vipi umoja wa taifa lenye makabila zaidi ya 40 utakuzwa, kila mmoja akiongea lugha yake ya mama?” aliuliza Dkt Noor.
Dkt Noor ambaye ni mwanachama wa chama kinachotetea ukuaji wa lugha ya Kiswahili cha Wakita, alisema hakuna ubaya wowote kuzungumza lugha za kiasili nyumbani na mashinani, lakini maswala ya utaifa ni lazima yakuzwe kuanzia bungeni, kwa kutumia lugha zinazokubalika kisheria na kikatiba.
“Kiswahili ndio lugha ambayo imetambuliwa kama lugha ya kitaifa. Kutumia lugha za kiasili katika bunge za kaunti itakuwa ni mbinu moja ya kuficha habari za ufujaji wa pesa, maovu ya kiuchumi na ukiukaji wa sheria,” alisema Noor.
Aliongezea: “Mtu ambaye ni Mluhya ataelewaje bunge la Nyeri linasema nini iwapo bunge hilo litazungumza kwa Kikuyu? Ni lazima tuongee lugha moja kama watu wamoja, watu wa Kenya.”
Wakati wa mkutano na wanahabari jijini Nairobi kuhusu agenda ya Cord siku ya Jumatano wiki jana, Raila alisema hana tatizo na wabunge wa kaunti wakizungumza lugha za kiasili, akisema hilo linafanyika hata Afrika Kusini ambapo lugha 11 za kiasili zimeidhinishwa kutumika.
“Ni kwa nini wawakilishi wadi wanaoketi katika bunge la Nyeri ambao wote ni Wakikuyu, wasiruhusiwe kutumia kikuyu, ama Bungoma ambao wote ni waluhya wasiruhusiwe kuzungumza kibukusu? Tunafaa kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu jambo hili,” alisema Raila.