Viongozi wa kisiasa katika ukanda wa Pwani wamedai kutopitisha sheria za ardhi zisizokuwa na manufaa yoyote kwa wakenya na hususan kwa wakazi wa Pwani.
Wakiongozwa na Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa Mishi Mboko, Wabunge hao wamesema kwamba watahakikisha kuwa miswada iliyo mhimu na yenye kumfaidi mkenya hususan wa eneo la Pwani ndio watakayoiunga mkono.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatano katika kongamano la wabunge wa Pwani la kujadili miswada ya ardhi ikiwemo ule wa dhuluma za kihistoria, Mishi alisema kwamba iwapo bunge litapitisha mswada huo, basi wakenya watasaidika pakubwa na dhuluma za unyakuzi wa ardhi na kufurushwa katika ardhi zao bila ya notisi wala fidia.
“Tumekubaliana kwa kauli moja kuungana na kupitisha miswada muhimu bunge itakayomfaidi mkenya na hususan mkaazi wa pwani ili kuona kwamba maswala ya mzozo ya ardhi inatatuliwa vyema kwa kuhakikishwa kuwa mswada wa dhulma za kihistoria unapitishwa bila pingamizi bungeni,” alisema Mishi.
Aidha amesema kwamba wabunge wamekubaliana kwa kauli moja kuungana na kuhakikisha kuwa wanapitisha miswada muhimu bungeni ili kuona kwamba eneo hilo halikumbwi tena na mzozo ya ardhi kila uchao hasa wakazi wa ukanda wa Pwani.
Wakati huo huo amekashfu hatua ya baadhi ya wabunge kuwasilisha mswada bungeni wa kuivunjilia mbali tume ya kitaifa ya ardhi nchini, NLC, na kuipa mamlaka zaidi Wizara ya Ardhi nchini kwa madai kuwa tume hiyo imeshindwa kuwajibikia majukumu yake kikamilifu.
Kauli ya viongozi hao imejiri baada ya vuta ni kuvute kulikumba bunge la kitaifa kuhusu mswada wa kuvunjilia mbali tume ya kitaifa ya ardhi pamoja na kusimamishwa kazi makamishna wa tume hiyo kutoafikiana vyema wabungeni.