Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa mrengo wa Jubilee katika Kaunti ya Mombasa Ali Mwatsahu ameunga mkono kauli ya Rais Uhuru Kenyatta ya kukosa kutoa nyongeza ya mishahara ya walimu ya aslimia 50 hadi 60.

Akiongea katika mkutano wa mrengo huo mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mwatsahu alisema kwamba mishahara ya walimu haipaswi kuongezwa na iwapo serikali itatoa nyongeza hiyo kwa walimu, basi huenda gharama ya maisha kwa mwananchi wa kawaida ikaongezeka.

Mwatsahu alisema kwamba ni jukumu la miungano ya vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini Knut na Kuppet kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo kwa taifa hili na kusema kwamba migomo ya kila mara hudidimiza uchumi wa taifa.

“Rais Kenyatta amechukua hatua mwafaka zaidi kwani gharama ya maisha itaongezeka iwapo walimu watapewa nyongeza. Hatutakubali walimu waongezwe mishahara kwani serikali kwa sasa haina pesa za kugharimu nyongeza hiyo walimu wanayodai,” alisema Mwatsahu.

Mwanachama wa muungano wa vyama vya kutetea haki za wafanyikazi nchini Patrick Mwangale aliunga mkono kauli ya Mwasau na akaukashifu upande wa upinzani wa mrengo wa Cord kwa kuingiza siasa katika suala la mgomo wa walimu.

“Serikali inatekeleza jukumu lake jinsi ipaswavyo na iwapo walimu basi watakubali kuingizwa siasa tume ya kuajiri walimu ichukua jukumu la kuwafuta kazi,” alisema Mwangale.

Kauli ya viongozi hao imejiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusema kwamba serikali haiwezi mudu gharama ya walimu ya nyongeza ya mishahara na marupurupu wanayodai, na kuwashikinikiza walimu kurudi shuleni.