Waziri wa Ardhi, Mkao na Mipangilio ya mji katika kaunti ya Mombasa Francis Thoya amelitaka bunge la kitaifa kuivunjilia mbali tume ya kitaifa ya ardhi nchini kwa kushindwa kutatua kesi za mizozo ya ardhi nchini.
Kulingana na Thoya, serikali ya kaunti ya Mombasa iliwahi wasilisha kesi zaidi ya 700 tangu mwaka wa 2013 kwa tume hiyo, lakini hakuna kesi hata moja iliwahitatua na kutafuta usawa kwa wananchi ili kuona kwamba mizozo ya ardhi inasitishwa.
Akiongea katika kongamono la wadau mbalimbali wa maswala ya ardhi nchini walio kongamana mjini Mombasa siku ya Jumatano, Thoya alisema kwamba hali hiyo inatokana na kuzembea kwa majukumu ya makamishna wa tume hiyo na iwapo itavunjiliwa mbali, huenda kukawa na mabadiliko nchini.
“Sio kama kuna haja ya kutengemea tena tume ya kitaifa ya ardhi nchini kwa sababu imeshindwa kutatua mizozo ya ardhi kaunti kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla. Tumewahi wasilisha kesi za mizozo ya ardhi ikiwemo unyakuzi wa ardhi lakini hakuna hata kesi moja tume ya ardhi ilitatua, sasa haina umuhimu kwetu tena,” alisema Thoya.
Thoya alisema kwamba bunge linafaa kujadili kwa kina miswada miwili tata ya ardhi iliyoko bungeni ukiwemo ule wa mswala ya haki za kihistoria ili kuleta mabadiliko katika maswala ya ardhi kwani wakazi wamepoteza matumaini na tume ya kitaifa ya ardhi nchini.
Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi, aliyesema kwamba iwapo bunge litashindwa kuivunjilia mbali tume hiyo, basi wananchi wataenda mahakamani kushinikiza kubanduliwa kwa makamishna wote wa tume hiyo na kuchaguliwa wengine.
“Iwapo bunge la kitaifa itashindwa kuivunjilia mbali, basi sisi tutaelekea mahakamani na kuishinikiza mahakama iwabandue makamishna wa tume hiyo na kuchaguliwe wengine kwani wameshindwa kabisa tutatua mizoz ya ardhi huku tukiona wakazi wakinyanyaswa,” alisema Mwinyi.
Mchakato huo umejiri siku chache tu baada ya spika wa bunge la kitaifa nchini Justin Muturi kupokea mswada wa kuivunjilia mbali tume ya kitaifa ya ardhi na mamlaka ya tume hiyo kukabidhiwa wizara ya ardhi nchini.
Mkuu wa ardhi, makao na mipangilio ya mji katika kaunti ya Mombasa Francis Thoya. Alisema kwamba kama viongozi wa kaunti ya Mombasa kuhusu maswala ya ardhi hawanaimani tena na tume ya kitaifa ya ardhi nchini na kupendekeza ivunjiliwe mbali.