Mwenyekiti wa Baraza la Mashauri ya Kiislamu nchini KEMNAC Sheikh Juma Ngao amewataka viongozi wa serikali ya Kaunti ya Mombasa pamoja na Kamishna wa kaunti hiyo kuwashinikiza viongozi wa bandari ya Mombasa KPA kuajiri vijana.
Akizungumza mjini Mombasa Siku ya Ijumaa, Sheikh Ngao alisema kuwa vijana wengi wamejitosa katika uraibu wa utumizi wa dawa za kelevya na uhalifu kutokana na ukosefu wa ajira na akawataka viongozi hao kuingilia kati swala hilo na kuwajiri vijana wa kaunti ya Mombasa.
“Wasimamizi wa Bandari ya Mombasa walisema watawaajiri vijana elfu moja baada ya kujengwa sehemu mbili za kuegesha meli. Tumeona hilo wamelifanya lakini bado vijana hawana kazi,” alisema Sheikh Ngao.
Kiongozi huyo wa kidini amewashinikiza viongozi na wasimamizi wa Bandari hiyo kuweka wazi shughuli zao ili kuhakikisha vijana wa Kaunti ya Mombasa wanafaidika na raslimali ambazo ziko katika kaunti hiyo.
Ngao alisema kuwa bila ya swala hilo kuangaziwa, basi vijana wengi watajiunga na uhalifu.
“Wakuu wa bandari ya Lamu pia walisema watatoa ajira lakini bado vijana wanarandanranda mtaani na hilo ni tishio kubwa kwa usalama kwani vijana hawa wanawezajiunga na uhalifu kutokana na ukosefu wa ajira,” aliongezea Sheikh Ngao.