Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kidini pamoja na wakazi wa eneo la Pwani wametakiwa kuungana kudumisha amani, uiano na utangamano ili taifa liwe na usalama.

Akiongea baada ya ibada ya kusheherekea sikukuu ya Eid-al-Adha siku ya Alhamisi mjini Mombasa, Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar alisema kwamba Kenya ina makabila zaidi ya 42 na iwapo watu wataanza kutengana na kubaguliana kwa misingi ya kikabila, kidini na kisiasa, basi hakuna hatua zozote za kimaendelea zitatekelezwa.

Omar amewataka wakenya kuungana na kuliombea taifa hili ili kuona kwamba wananchi wanaishi kwa amani na bila changamoto zozote za ukosefu wa usalama.

“Ni jukumu la wakenya kuungana pamoja na kuliombea taifa hili ili kuwa salama kwani kubaguliana kila uchao kwa msingi ya kikabila, kidini na kisiasa kamwe hautasaidia taifa hili kusonga mbele kimaendeleo.Kwa hivyo, wakenya tuungana na kudumisha amani,” alisema Omar.

Mbunge wa Mvita Sharrif Nassir alisema kwamba ni jukumu la jamii ya Kiislam kujitenga na migawanyiko na badala yake kuhimiza uiano pasipo na kuzingatia misingi ya kidini, kikabila wala kisiasa.

“Tafadhili Waislamu tusikubali kugonganishwa na baadhi ya watu Fulani na kuzua vurugu kisha kugawanyika. Tafadhilini ndugu zangu tuungane na tuzidi kuwahimiza viongozi watekeleza majumu yao ya kuwafanyia wakenya maendeleo mashinani,” alisema Nassir.

Kauli ya viongozi hao wa kisiasa iliungwa mkono na waumini waliyohudhuria ibada hiyo maalum kabla ya kuanza sherehe za shamra shamra za sikukuuu hiyo.