Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku suala la ardhi likiwa lenye zogo kuu miongoni mwa umma katika maeneo mengi nchini, Wakazi pamoja na viongozi wa kisiasa kutoka katika eneo zima la pwani wametakiwa kuungana mkono na kupinga mswada ambao utaletwa bungeni kuhusiana na masuala ya ardhi.

Kulingana na kiongozi wa muungano wa upinzani wa Cord bwana Raila Odinga, mswada huo unalenga kuwadhulumu wakazi wa maeneo ya pwani ambao ndio wameathiriwa na unyakuzi wa mashamba yao tangu nyakati za kupata uhuru wa nchi hii ya Kenya.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Bahari Benedict Fondo alisema kuwa serikali pamoja na baadhi ya viongozi wa Jubilee wana nia ambayo inalenga kunyanyasa wenye ardhi nchi hasa wakazi wa pwani ambao wamekuwa wakidai haki ya mashamba yao ambayo yalichukuliwa na wanasiasa kwa njia za kutiliwa shaka.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema kuwa serikali ina mpango wa kurejesha usimamizi wa mashamba kwenye mikono ya serikali ilhali katiba mpya ilishawapa umma mamlaka ya kusimamiwa kwa ardhi za umma kupitia kwenye sheria ya ugatuzi hivyo ardhi yote ya umma itabakia kusimamiwa na serikali za kaunti.

Mswada huo ambao huko katika awamu ya mwanzo ya kujadiliwa katika bunge la taifa ni mojawapo ya juhudi za wizara ya ardhi kuona kuwa inakuwa na udhibiti wa moja kwa moja katika ardhi nchini.