Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amewataka viongozi wa makanisa kutoka kaunti hiyo kushirikiana na kuwashauri vijana dhidi ya kujihusisha na makundi ya ugaidi.
Akiongea katika shule ya upili ya Kiseminari ya St. Benedict Kisii, kwenye hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, Maangi aliwasihi wanafunzi kukumbatia maadili ya bibilia na kuepuka makundi ambayo huwapotosha kwa kuua wenzao ili kupata pesa kutoka kwa makundi haramu kama ya Al Qaida na yale ya Al Shabaab.
Maangi ambaye pia ni mwanakamati mkuu wa wa Kamati ya Manaibu wa magavana nchini Kenya, aliwasihi viongozi wa makanisa na wale wa Kiislamu kukaza misuli kwa kuwajuza vijana njia mwafaka na zile za kiroho, huku akifunua kuwa wengi wa vijana ambao hujiunga na makundi ya kigaidi hukosa mwelekeo mwema na baadhi hutengwa na jamaa zao, hali ambayo huwasukuma kufanya lililo hiari kwao.
Kwingineko, naibu huyo aliitaka serikali kuu kuzipa serikali za kaunti mamlaka ya kuendeleza shule kwani wao ndio wako karibu na shule hizo.
Aidha, aliwashukuri walimu kwa ushirikiano uliopo baina yao na serikali za kaunti, na vile vile kuwataka wasimamizi wa shule kuwaongoza wanafunzi kwa kuwapa ushauri nasaha wanaposhuku tatizo miongoni mwa wanafunzi wao.