Kufuatia agizo la kaunti ya Kisii kuwataka viongozi wa makanisa pamoja na wahubiri kulipia uga wa michezo wa Gusii takribani shilingi elfu tatu kila siku ili kuandaa hafla yeyote, baadhi ya viongozi wa makanisa wamekashfu hatua hiiyo.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii, mhubiri Japhet Moruri, ambaye ni mwijilisti wa kanisa la God iS Faithful Ministries, amesema kuwa ada hiyo ya takribani shilingi elfu tatu kila siku ni ghali mno, na sharti msuada huo uangaliwe upya ili kuwafanyia haki watumishi wa Mungu.
Aidha, aliongezea kuwa makanisa mengi hayana ufadhili wowote, na hela ambazo wanapata ni mchango kutoka kwa waumini wa kanisa husika.
Moruri aliongezea kusema kuwa kwa serikali ya kaunti ya Kisii kuanza kuwatoza ada kiasi kikubwa kama hicho ina maana kuwa wengi wa watumishi na wainjilisti wahiari kufunga madhabahu kwa kukosa uwezo wa kulipa hela hizo.
Alitoa wito kuwa serikali iangalie hela hizo labda zitozwe kila wiki au kuweka kiwango angaa mia tano kwa kila siku ya ibada itakuwa nafuu kwao.
“Kiwango kama hicho cha hela kinalenga kumaliza injili na makanisa hayataweza kuhudumu kwa makanisa ufadhili na waumini husika wa kanisa, hivyo naiomba serikali yetu ya kaunti kuweka kiwango ambacho kanisa litakimu kulipia,” alisema Moruri.
Wito kama huu ulitolewa siku ya Jumatano wakati wa umma kushiriki kutoa maoni yao kwenye msuada huo wa fedha wa bunge la kaunti, ambapo mmoja wa viongozi wa makanisa, Mosomi Isaboke alitoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Kisii kupunguza kiwango hicho kilichopendekezwa.