Mbunge wa eneo bunge la Bomachoge Borabu amewaomba viongozi wote wa Kaunti ya Kisii kuungana ili kuleta maendeleo.
Akiongea siku ya Jumatatu katika shule ya wasichana ya Omobera, alipohudhuria mkutano wa kuchagua wasimamizi wa bodi ya shule hiyo, Joel Onyancha aliwaomba wanasiasa kuweka kando masuala ya kisiasa na kugombana kila wakati na kufanya maendeleo kwa wananchi wa kaunti hiyo kwani walichaguliwa kufanya maenendeleo.
Mbunge huyo alisema kuwa kile wakazi wa Kaunti ya Kisii wanachohitaji ni maendeleo wala si siasa za hapa na pale.
Haya yanajiri baada ya kusemekana kuwa Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae na naibu wake Joash Maangi wametofautiana jambo ambalo mbunge huyo alisema ni la kushangaza mno kwani walichaguliwa na wananchi kufanya maendeleo pamoja kama viongozi wa kaunti.
“Naomba Gavana Ongwae na naibu wake Maangi walete maendeleo kwa wananchi wa Kaunti ya Kisii. Mlipochaguliwa mlichaguliwa pamoja na hukumu itakatwa na wananchi wa Kaunti ya Kisii kwa nyinyi nyote wawili sio mmoja wenu,” alisema Onyancha.
Mbunge huyo pia alitembelea shule mbalimbali za eneo bunge lake ili kuzikabidhi pesa za ustawi wa maeneo bunge ili kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo katika shule hizo.
Onyancha aliwaomba wasimamizi wa shule hizo kutumia pesa hizo vizuri na kuweka orodha ya matumizi ya pesa hizo.