Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa bodi ya shirika la kupambana na utumizi wa mihadarati na vileo nchini Nacada Sheikh Juma Ngao amewataka viongozi katika Kaunti ya Mombasa kuacha kuingiza siasa katika afya ya wananchi na badala yake kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata afya bora.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa facebook aliyochapisha siku ya Jumanne, Ngao alielezea kuwa tayari wameanza kazi ya kuwanasua waathiriwa wa dawa za kulevya katika kaunti ya Mombasa.

“Vita dhidi ya utumiaji wa dawa za kulevya tayari vimeanza na tutahakikisha kuwa waathiriwa wamepata nafuu kutokana na shughuli hiyo,” ilisoma sehemu ya taaarifa yake.

Bw Ngao pia aliwaomba wananchi waungane mkono ili kukabiliana na janga hilo ambalo linakita mizizi katika kaunti hiyo na kuwasihi waasi siasa zisizoleta maendeleo.

“Ombi langu ni tusiingize siasa katika kushughulikia afya ya wananchi. Hivyo basi, nawaomba tuungane pamoja ili kuhakikisha kuwa waathiriwa wa dawa za kulevya wanapata nafuu,” alisema Ngao.

Ngao aliwahakikishia wananchi kuwa eneo la Miritini la NYS litaanza kupokea baadhi ya waathiriwa kuanzia siku ya Jumatatu wiki ijayo kama ilivyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita.

Haya yanajiri siku moja baada ya mkurugenzi huyo kumwomba Rais Uhuru Kenyatta kuivunjilia mbali bodi hiyo kutokana na wakurugezi wakuu kushindwa kuwajibikia majukumu yao.