Maafisa wa polisi wilayani Nyamira wanaendelea kuchunguza kisa ambacho vipande vya mwili wa mwanamke vikiwemo mguu mmoja, sehemu ya kifua na matumbo, yalipatikana katika sehemu ya Charachani wilayani humo.
Akizungumza siku ya Jumapili afisa mkuu wa polisi wilayani Nyamira, bwana Rico Ngare, alisema mbali na vipande hivyo kupatikana, pia kulikuwa na sidiria na chupi ya mwanamke katika pahala pa tukio hilo.
Ngare aliongezea kuwa huenda washukiwa walitekeleza unyama huo kwingine na kutupa vipande hivyo vya mwili wa marehemu katika sehemu hiyo.
"Tumeanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hichi ambapo inaonekana kuwa washukiwa walitekeleza mauaji hayo kwingine na kutupa vipande hivyo katika sehemu hiyo, kwa sababu hakuna dalili inayoonyesha kutendeka kwa tukio hilo katika sehemu hiyo," alisema Ngare.
Aidha, Ngare aliongezea kuwa uchunguzi utabaini ukweli wa mambo, huku akiwataka wakazi waliompoteza jamaa wao kufika na kuripoti kwa kituo cha polisi kwa sababu huenda wakamtambua.
Alisema kuwa vipande hivyo vimehifadhiwa kwenye hifadhi ya Hospitali kuu ya Nyamira.
"Kufikia sasa hatujapata ripoti yoyote kuhusu mtu aliyepotea katika kituo chetu cha polisi. Nawaomba wananchi ambao wamempoteza mtu wao kufika na kuwasaidia maafisa wa polisi kwa uchunguzi zaidi," aliongezea Ngare.