Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mkuu katika Kituo cha Polisi cha Lari amesema kwamba kesi za wizi wa mabavu zimeongezeka kwa asilimia kubwa kwa muda wa mwezi mmoja.

Akizungumza ofisini mwake siku ya Ijumaa, Inspekta Mkuu Peter Ouko alisema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja,visa 12 vimeripotiwa katika eneo hilo.

Alisema kwamba visa hivyo vinashukiwa kuwa vinatekelezwa na kundi fulani la majambazi, na kuwaomba wazazi na wakazi wa eneo hilo kuwapa mwongozo mwema watoto wao ili kuwazuia kujiunga na kundi za aina hiyo.

Ouko alisema kwamba polisi walitekeleza msako mkali siku ya Alhamisi na waliweza kuwakamata vijana 11 ambao wanashukiwa kuwa wanatekeleza uovu huo.

Alisema kuwa visa hivyo vinatekelezwa kwanzia saa nne usiku na kuwaonya wale wanaoendeleza uhalifu huo akisema kuwa chuma chao ki motoni.

Ouko alisema kuwa amewapa wahalifu hao nafasi ya kuachana na uovu huo ama wote wachukuliwe hatua kali ya kisheria.

"Wizi wa aina hii ni wa kifungo cha miaka mingi gerezani na wale wanaotekeleza ni vijana wadogo ambao wana nafasi ya kubadilika na kuwa watu wa manufaa kwa jamii. Nawaonya waache shughuli hiyo ama sheria itawaandama," alisema Ouko.

Beth Wangari, mkaazi wa Lari, alisema kuwa wizi huo umeanza hivi majuzi na unaendelea kuwapa wakazi hofu.

Aliwaomba maafisa wa usalama kushika doria usiku ili kuwahakikishia wakazi usalama.