Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amewaomba walanguzi wakuu na watumizi wa dawa za kulevya kusitisha biashara hiyo haramu la sivyo mkono wa sheria utawaandama.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Marwa alisema kuwa serikali haitasitisha vita dhidi ya walanguzi wa mihadarati na akawaonya wale wanaodai kuwa serikali inatoa tu vitisho vya kuwakabili walanguzi wa mihadarati lakini hakuna hatua zozote zitachukuliwa.
Marwa alisema kuwa lazima wanaofanya biashara hiyo kukabiliwa kikamilifu huku akiwataka kusitisha biashara hiyo na kuanza biashara ya kuvua samaki na kusafirisha mahindi, kwani serikali itawaandama kila mahali watakapo kwenda kufanya biashara hiyo haramu.
“Ningependa kuwahakikishia wakazi kuwa hakuna siku serikali itaanza vita kisha ikifika katikati inashindwa. Upende usipende vita hivyo vitaendelea uwe ulanguzi mkuu, uwe nani utapigwa vita hata ukimbie wapi utapatikana tu,” alisema Marwa.
Kamishna huyo wa kaunti ya Mombasa amewahimiza wakazi, viongozi wa kidini na wale wa kisiasa kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama katika kutoa habari kuhusu walanguzi na watumizi wa dawa za kulevya ili watiwe nguvuni na kufunguliwa mashataka.
“Tunauliza wakazi wote, viongozi wa kidini na wale wa kisiasa kushirikiana na serikali na maafisa wa polisi pamoja na serikali ya kaunti ili tupate habari kuhusiana na wale wanaouza dawa hizo,” aliongezea Marwa.
Kauli ya Kamishna huyo imejiri baaada ya Rais Uhuru kenyatta kutangaza vita dhidi ya walunguzi wa dawa za kelevya humu nchini, hususan katika Kaunti ya Mombasa na eneo nzima la Pwani.