Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya vimepata pigo baada ya baadhi ya waraibu ambao walikuwa katika kituo cha kurebisha tabia cha Reachout Centre kurejeshwa makwao ilipobainika kuwa walikuwa wakiendelea na matumizi ya dawa hizo.

Madai yalizuka wiki jana baadhi ya waraibu walipodokeza kuwa wenzao walikuwa wakijihusisha kwenye matumizi ya mihadarati hata wakiwa kituoni ambacho kiko katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika hospitali hiyo mkuu wa idara ya afya katika kaunti ya Mombasa, Binti Omar, alisema kuwa wamechukua hatua hiyo ya kuwarejesha nyumbani kwa kukosa kujitolea na kutoonyesha ari na moyo wa kusaidika.

Alisema kuwa idadi ya waathiriwa ambayo kituo hicho kinashughulikia ni kubwa mno na imekuwa changamoto hasa kuhusiana na kiwango cha pesa ambacho wanalipa kumhudumia kila mwaathiriwa ambaye yumo kituoni.

"Imekuwa changamoto kubwa kugharimia matibabu ya waathiriwa wa dawa za kulevya na hela ambazo zinahitajika kuwahudumia ni nyingi ikizingatiwa idadi ambayo tunashughulikia ni zaidi ya mia moja hamsini na bado msaada wa kifedha hautoshelezi," alisema Omar.

Haya yanatokea huku kukiwa na misururu ya watumiaji wa dawa za kulevya kutoroka vituoni na wengine kufurushwa kwa kukosa kuzingatia masharti, ambapo visa ambavyo vimechangia hayo ni baadhi ya watumiaji ambao walikuwa sugu kushindwa kukabiliana na hali ya kukaa bila kutumia mihadarati.