Share news tips with us here at Hivisasa

Wawakalishi 66 wa bunge ya kaunti ya Kisii walisusia kikao chao siku ya Jumanne kufuatia kutolipwa kwa marupurupu na kulazimu spika wa kaunti hiyo Kerosi Ondieki kuhairisha vikao hivyo hadi siku ya Jumatano mchana.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumanne nje ya jengo la bunge hilo lililoko katika mji wa Kisii, spika huyo alisema kuwa kati ya wawakilishi 71 ni wawakilishi wanne pekee waliohudhuria kikao cha jana.

Ondieki alisema kulikuwa na masuala muhimu ya kujadiliwa katika bunge hilo lakini akalazimika kuhairisha vikao hivyo kufuatia upungufu wa wawakilishi katika bunge hiyo ya kaunti ya Kisii.

“Vikao havingeweza kuendelea kwa sababu hakukuwa na wawakilishi wa kutosha ili kujadili masuala ya bunge,” alisema Ondieki.

Kufikia sasa ripoti kamili imetolewa ambayo inasema kuwa bunge la kaunti ya Kisii ilitumia pesa nyingi zaidi ya kiwango kile serikali ya kaunti hiyo inastahili kutumia na kuwasababishia wabunge wa kaunti hiyo kutopata marupurupu yao kwa muda ufaao.

Bunge la kaunti ya Kisii lina wawakilishi 71. Wawakilishi 45 walichaguliwa kutoka wadi zao na wengine 26 waliteuliwa na bunge hilo.