Wabunge wanaowakilisha maeneo ya Mlima Kenya wametupilia mbali hoja ya kuleta katika bunge la taifa kumtimua kiongozi wa walio wengi Bw Aden Duale.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hapo awali Wabunge hao walikuwa wametisha kuwasilisha mswada huo kufuatia kukithiri kwa mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya Kaskazini Mashariki na walimlaumu Duale kwa kutotoa orodha ya wafadhili wa ugaidi nchini.

Hata hivyo, wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega walisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya majadiliano ya kina kutoka pande zote mbili.

Kega alisema kuwa wanapanga kuleta mswada mwingine bungeni utakao lenga kunufaisha jamii zinazoathiriwa na visa vya ugaidi kwani watapewa fidia ya Sh5 milioni kila mmoja.

"Tunatarajia kuleta mswada mwingine utakaolenga kuzifaidi jamii zinazoathirika na ugaidi," alisema Mbunge Kega na kuongeza kuwa hatua hiyo itaisukuma serikali kuu ili kukabiliana vilivyo na ugaidi nchini.