Wabunge wanne kutoka jamii zinazojihusisha na ufugaji nchini wamekashifu hoja ya kumtimua kinara wa walio wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale.
Wabunge hao ambao walikuwa wakizungumza katika shule ya upili ya Olderkesi katika Kaunti ya Narok waliwasuta wenzao wa TNA kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakitishia kuwasilisha mswada bungeni ili kumtimua Duale kwa kukosa kutoa orodha ya wanaojihusisha na kufadhili juhudi za kundi la Al Shabaab nchini.
Wabunge hao wakiongozwa na mbunge wa Turkana Kusini James Lomenen walidai kuwa wanaotaka kumwondoa Duale bungeni wanafanya hivyo kwa sababu za kibinafsi.
Lomenen alisema kuwa kinara huyo ameridhisha katika utendakazi wake kama kinara wa walio wengi na watafanya kila juhudi ili kuupinga mswada wa kumtimua.
"Duale amefanya vizuri sana katika wadhifa wake wa kinara wa walio wengi na wanaotaka ang'atuke ni sharti watathmini tena jambo hilo," alisema Lomenen.
Wabunge wa eneo la Kati walikuwa wametishia kumtimua Duale kufuatia kukithiri kwa mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa na Al Shabaab sehemu za Kaskazini Mashariki ambayo yaliwaua wengi kutoka kaunti zao.
Wabunge wengine waliokuwepo katika hafla hiyo ni Patrick Ntutu wa Narok Magharibi, Korei Lemein wa Narok Kusini na Protus Akuja wa Loima.