Pana haja kwa serikali za kaunti kujenga soko za kisasa ili kuimarisha biashara miongoni mwa wananchi.
Mbali na kuwa hali hiyo itaimarisha biashara na kuinua uchumi wa nchi, kufanya hivyo pia kutawahakikishia wachuuzi usalama katika soko nyingi nchini. Hii ni ikizingatiwa kuwa baadhi ya wachuuzi hulazimika kuuza barabarani hali ambayo huchangia ongezeko la ajali ambako wafanyibiashara hawana soko maalum.
Licha ya hali kuwa hivyo kwa muda mrefu, halmashauri ya manispaa ya miji imeendelea kukusanya ushuru kwa wafanyibiashara hao bila kujali mazingira yao mabaya.
Katika Kaunti Ndogo ya Muhoroni, soko nyingi za mashinani wachuuzi huonekana wakimiminika kandokando mwa barabara, huku magari na mashine nyingi zinazotumia barabara hizo zikilazimika kusimama zifikapo maeneo hayo.
Soko za Oseng'tet na Koru zilizoko barabara za Chemelil na Muhoroni, hakuna hatua ambayo imechukuliwa kuwapa wafanyibiashara mazingira bora ya kazi, licha ya kuweko lalama kutoka kwao wakitaka kujengewa soko katika maeneo hayo.
Hata hivyo, pia pana haja ya halmashauri za miji kuweka mikakati mwafaka ya kuelekeza wachuuzi wanaoendesha biashara zao kandokando mwa barabara, kuweka bidhaa zao mbali na barabara hatua zinazotakikana kulingana na sheria za trafiki nchini.