Wachuuzi wa kuuza bidhaa mbalimbali katika mji wa Nyamira wameomba serikali ya kaunti ya Nyamira kuwajengea vibanda ili waweze kukuza biashara zao.
Wakiongea na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika mji wa Nyamira, wachuuzi hao waliomba serikali kuwajengea vibanda katika mitaa yote ya mji huo kwani kwa sasa wanauzia bidhaa zao mahala palipo wazi.
“Tunaomba Gavana wetu wa kaunti kutukumbuka sisi wachuuzi na kutujengea vibanda ili tuwe tunajikinga wakati mvua inaponyesha na hata kuzuia bidhaa zetu kuchafuliwa na vumbi kila wakati,” alisema Justine Ombwori mchuuzi.
Wakati huo huo, wachuuzi hao walisema watafurahia sana ikiwa watakumbukwa na serikali kama sehemu zingine za kaunti hiyo kwani kuna baadhi ya sehemu ziko na vibada hivyo.
“Tutashukuru sana tukijengewa vibanda hivyo, ata vya mabati ili tuwe tunajizuia na mvua na tutakuza biashara zetu bila changamoto yoyote maana mvua inaponyesha tunahama na tunarudisha bidhaa zetu tunapouzia,” alisema Omwanza Peterson, mchuuzi mwingine.
Kwa sasa ni serikali ya kaunti imebaki na ombi hilo ambalo wengi wanatarajia kushughulikiwa kwa wakati ufahao maana ni jukumu la serikali kufanya hivyo, haswa sekta hiyo ya kushughulikia soko kwani sekta nyingi zililetwa kuwa chini ya uongozi wa kaunti.