Waendeshaji bodaboda katika wadi ya Ojola iliyoko Kisumu Magharibi, wameitaka serikali ya kaunti hiyo kukarabati barabara za eneo hilo.
Wakiongea siku ya Alhamisi kwenye hafla ya harambee ya Ojola Bodaboda Sacco, wahudumu hao walimtaka mwakilishi wa wadi hiyo, Charles Dimo kuangazia swala hilo katika bunge la kaunti.
Wahudumu hao walielezea hasara wanayopata kutokana na barabara mbovu za eneo hilo.
Walidokeza kwamba sehemu nyingi za barabara hizo zilichimbuka na zina mashimo mengi ambayo hayapitiki kwa urahisi, hali ambayo huwalazimu kutumia mafuta mengi kwenye pikipiki zao, huku wakihitajika kuzirekebisha kila mara.
''Huwezi tumia pikipiki wiki mzima kabla haijaharibika kitu kinachohitaji pesa nyingi ndipo kirekebike,'' alisema mwenyekiti wa kundi hilo, Sam Makunga.
Aidha, walisema kwamba barabara za eneo hilo zilikuwa zimekarabatiwa hapo awali, lakini ziliaribika baada ya mvua kubwa ya masika ambayo ilinyesha msimu uliopita.
Tangu kuwepo kwa serikali za ugatuzi nchini, waendeshaji bodaboda katika maeneo mengi ya Kaunti ya Kisumu wamekua katika mstari wa mbele kushinikiza serikali kukarabati barabara na kuwajengea vivuli na maeneo ya kuegeza pikipiki zao.