Waendeshaji bodaboda wa kituo kilichoko katika soko la Magenche, eneo bunge la Bomachoge Borabu kaunti ya Kisii wamemshukuru mwakilishi wa wadi hiyo ya Magenche, Ogugu Timothy kwa kuwakabidhi mabati ya kujenga kibanda ambacho wamekuwa wakisubiri kujengewa kwa muda mrefu.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika soko la Magenche, baada ya mwakilishi huyo kuwakabidhi mabati hayo, waendeshaji bodaboda hao walimshukuru mwakilishi huyo kwa kuwakumbuka kwani wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu kutokana na mvua inayoendelea kunyesha katika sehemu za Kisii.
Mwakilishi wetu ameleta maendeleo na tunasema asante kwa hayo mabati ametupatia ili tujengewe kibanda katika eneo hili kwani tumekuwa tukisumbuka sana kutokana na mvua,” alisema Peter Onsarigo, mwendeshaji bodaboda.
“Tunaomba mwakilishi wetu aendelee kusaidia waendeshaji bodaboda wengine katika wadi hii ili kila kituo kiwe na kibanda chao. Tumeona kuwa mwakilishi huyu anajali maslahi yetu kama waendeshaji wa bodaboda,” alidokeza Anderew Obare mwendeshaji bodaboda.
Wanabodaboda hao wamekuwa wakisumbuka sana kutokana mvua na wakati mwingine kutokana na jua kali kwa muda mrefu. Sasa kilio chao kimeweza kusikika na mwakilishi wao jambo ambalo lilionekana kuwafurahisha sana.
Aidha, waendeshaji bodaboda hao waliahidi kuzingatia sheria za barabara wanapoendesha pikipiki zao jinsi walivyoombwa na mwakilishi wao alipokuwa anawakabidhi mabati hayo.