Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyabiashara wa soko marufu la Marikiti mjini Mombasa wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuwapa maafisa wao vitambulisho maalumu vya kuwatambulisha mbali na kuvaa sare zao pekee.

Wahudumu hao wa Marikiti wamedai kuwa baadhi ya maafisa ambao hukusanya ushuru hukosa kujitambulisha hata wanapombwa kufanya hivyo na wahudumu na wafanyabiashara, hali ambayo wanasema huwatia shaka wafanyabiashara ikizingatiwa kuwa baadhi ya masoko kwenye jiji hilo yameshuhudia watu ambao hulaghai wafanyabiashara kwa kizingizio kuwa wao ni maafisa wa kukusanya ushuru kutoka kaunti ya Mombasa.

Akiongea mjini mombasa kwa niaba ya jumuia ya wafanyabiashara siku ya Jumapili, naibu mwenyekiti wa wasambazaji na wauzaji wa bidhaa kwenye soko hilo Ahmed Swaleh, alisema kuwa itakuwa rahisi kwa wengi wa wafanyabiashara wanaohudumu si tu kwenye soko hilo bali masoko yote yaliyo kwenye kaunti hiyo kuweza kutambua ni nani afisaa halali.

Swaleh alifafanua umuhimu wa kuwa na vitambulisho hivyo na kusema itasaidia kaunti ya Mombasa kukusanya ushuru kutoka kwa wafanyabiashara na kusaidia kuwapa wakazi huduma za kuridhisha.

“Hii pesa ambayo inakusanywa na matapeli na walaghai ambao wengine wao hatuwajui ingetumiwa kwenye maendeleo ya kaunti yetu, na naiomba serikali ya kaunti kuwapa mafisa wao vibali na vitambulisho maalumu ili iwe rahisi kuwatambua haramu na wale halali kwenye idara ya kukusanya ada kutoka kwetu sababu hatujui nani ndiye nani,” alilalama Swaleh.