Ugawaji usio kuwa kisheria wa soko kuu ya Mwembe Tayari mjini Mombasa bado utabaki kuwa kitendawili baada ya tume ya kupiga vita dhidi ya ufisadi kufunga faili iliyomhusisha gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho kuwa alihusika katika kupewa kwa ardhi hiyo kwa wawekezaji binafsi.
Sasa wakazi pamoja na wafanyabiashara wa soko hilo wameitaka tume ya EACC kutositisha juhudi za kupata mhusika katika unyakuzi wa soko hilo.
Soko hilo ambalo ni la zamani na miongoni mwa masoko ya kitalii katika mji huo wa kale, na ambalo lilidaiwa kugawanywa na kupewa watu binafsi, limekuwa na mzozo, na ilibidi tume ya kupigana na ufisadi nchini EACC kuingilia kati na kuanza kumchunguza gavana Joho.
Kulingana na baadhi ya wafanyabiashara ambao waliongea na mwandishi habari huyu, walimtaka mkurugenzi mkuu wa EACC kukaza juhudi na kuwatafuta watu ambao huenda walichangia baadhi ya sehemu ya soko hilo kunyakwa.
Wakiongozwa na Salim Chengo, ambaye ni mwenyekiti wa wauzaji na wasambazaji wa mboga kwenye soko hilo alisema kuwa soko hilo ni la kitamaduni na huwa linachangia pato kubwa la kitalii kwenye kaunti hiyo, na ni sharti tume ya ufisadi itie bidii kutafiti na kuchunguza zaidi wahusika.
“Tunashukuru kuwa gavana wetu hakuhusika katika suala la kugawa soko hili na kunyakuliwa kwake, lakini bado tume ya EACC isisitishe vita vya wanyakuzi si tu soko hili bali ardhi zote za umma katika kaunti hii yetu,” alisema Chengo
Kesi ya gavana huyo imeweza kutupiliwa mbali baada ya uchunguzi kufanywa na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kuhusiana na kunyakuliwa soko hilo, ambapo mkurugenzi wa tume hiyo ya EACC Bwana Keriako Tobiko ameamurisha kufungwa kwa faili za kesi hiyo siku ya Jumatano.