Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyakazi wa Kaunti ya Kisii waliokosa kulipwa mishahara yao, wameombwa kuwa na ustahimilivu mpala kesi waliowasilisha katika mahakama kuu ya Kisii isikizwe na kuamuliwa.

Akiwahutubia wahudumu hao siku ya Jumatano nje ya afisi kuu za kaunti ya Kisii, mwakilishi wa Bassi Masige, Henry Moracha, alisema kuwa ni kinyume na sheria kushughulikia jambo ambalo liko mbele ya mahakama na sharti wafanyakazi hao wazingatie mwafaka wa katiba na sheria za kazi.

"Nawaomba mume na subira tungoje mahakama iamue kesi hii. Nawahakikishia kuwa nitapigania haki yenu ili muweze kupata pesa zenu," alisema Moracha. 

Mwakilishi wa wadi ya Boochi ambaye alijitokeza kuwazungumzia waandamanaji hao, Shem Ondara aliwatetea wafanyakazi hao kwa kusema kuwa ni kinyume na sheria kaunti kukosa kuwalipa wahudumu hao kwa miezi kumi sasa kwani wafanyakazi hao nao wana familia za kulisha.

Hata hivyo lawama zimekuwa kwa upande wa wawakilishi wa wadi wa kaunti hiyo ambao wanasemekana kusababisha zogo hilo baada ya kudaiwa kuleta watu na kutaka wapewa kazi na serikali ya kaunti ya Kisii bila kufuata utaratibu wa sheria.

Utata ulizuka baada ya serikali ya kaunti kudai kuwa wafanyakazi hao ni wengi mno kupita idadi ya watu ambao walikuwa wamethibitishwa rasmi na utawala wa kamati ya kushughulikia wafanyakazi wa kaunti. 

Hata hivyo juhudi za wahudumu hao kutaka kuhutubiwa na spika wa kaunti hiyo, Kerosi Ondieki hazikufanikishwa kwani inaidaiwa kuwa spika huyo hakuwa katika ofisi yake wakati wa maandamano hayo.