Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya msako ulioendelezwa dhidi ya meli kutoka nchini India ambayo ilishukiwa kuwa na mihadarati, imethibitishwa kuwa utaratibu wa kazi umerejelea kawaida kwenye bandari kuu ya Mombasa.

Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Ijumaa, mkurugenzi wa shirika la bandari nchini, Gichiri Ndua, alisema kuwa wafanyakazi kwenye vitengo vyote bandarini wamerejea kazini na kuwataka kutokuwa na shaka na shughuli ambayo ilikuwa inaendelezwa na vikosi vya polisi wa kupigana na mihadarati na Reke.

Licha ya msako huo ambao uliwaacha wafanyakazi wengi na mshangao na kushindwa kilichokuwa kikiendelea baada ya kuamrishwa kuenda nyumbani siku ya Alhamisi, bado haijabainika iwapo kile kilichoshukiwa kuwa kwenye meli hiyo kimepatikana.

Hata hivyo, shughuli za kazi zilikuwa shwari bandarini ila baadhi ya wafanyikazi waliitaka serikali kuwa na utaratibu mzuri wa kuendesha misako yao.

“Ni vizuri kufanya msako dhidi ya ugaidi na mihadarati lakini wakati mwingine, sharti tupewe ujumbe sababu baadhi yetu tulishtukia tu kuna msako. Hatahivyo, nashukuru kwamba tumerejelea kazi kama kawaida na tunaipongeza serikali kwa juhudi za kupambana na mihadarati na ugaidi hapa kwentu,” alisema Allan Mwelu, mfanyakazi katika bandari hiyo.