Wafanyibiashara katika eneo la Kabete wamelalamikia kuongezeka kwa watoza ushuru bandia katika eneo hilo jambo ambalo limefanya wasusie kutoa ushuru.
Akizungumzia swala hilo, mwenyekiti wa wafanyibiashara Kabete, Bwana Erastus Njuguna alisema kwamba walaghai katika eneo hilo wamezidisha mbinu zao kwa kujifanya watoza ushuru na kutembea katika biashara za watu wakidai ushuru.
Alisema kwamba walaghai hao pia wana sare bandia na risiti ambazo wanatumia ili kuhakikishia wafanyi biashara kwamba ni watoza ushuru.
Njuguna alisema kwamba wafanyibiashara wamesusia kutoa ushuru mpaka jambo hilo lishughulikiwe ili walaghai hao wakamatwe.
"Ulaghai umekiuka mipaka katika eneo la Kabete na tunataka swala hili kushughulikiwa vilivyo," alisema Njuguna.
Teresia Wamaitha, mfanyibiashara katika eneo hilo alisema kwamba walaghai hao ni vijana barubaru na kwa muda wa miezi minne sasa, wafanyibiashara wamekuwa wakiwapa pesa wakifikiri kwamba ni watoza ushuru.
Alisema kwamba jambo hili limewakasirisha kwa kuwa wamekuwa wakilaghaiwa pesa ambazo wanatafuta kwa bidii.