Mwakilishi wa Wadi ya Nyamaiya, Laban Masira, amewaonya vijana dhidi ya kuzua vurugu kwa madai kwamba serikali ya kaunti haijakuwa ikiwapa wafanyibiashara katika Soko la Miruka huduma muhimu.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza na mwandishi huyu katika mahojianao kwa njia ya simu siku ya Jumanne, Masira alisema kuwa wafanyibiashara katika soko la Miruka wamekuwa wakisusia kulipa ushuru kwa serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa kudai kuwa serikali ya kaunti hiyo haijakuwa ikitoa huduma muhimu kwao.

"Kwa wiki mbili sasa wafanyibiashara katika soko la Miruka wamekuwa wakisusia kulipa ushuru kwa serikali ya kaunti ya Nyamira kwa madai kwamba hawajakuwa wakipokea huduma muhimu. Nawaomba waendelee kulipa ushuru huku serikali ya kaunti ikijitayarisha kuweka mikakati kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa," alisema Masira.

Masira ambaye pia ni mwakilishi wa walio wengi kwenye bunge la Kaunti ya Nyamira alisema kwamba tayari Gavana John Nyagarama ameahidi kuhakikisha kuwa vyoo vya kisasa vimejengwa katika soko hilo, pamoja na kuhakikisha kuwa kuna maji yakutosha yatakayo tumika kwenye vyoo hivyo.

Akizungumzia swala lakufunguliwa kwa barabara zinazopita nyuma ya soko hilo, Masira alisema kuwa tayari masaroveya wameenda kukagua na kubaini mahali ambapo barabara hizo ambazo zimenyakuliwa na baadhi ya wakazi zilikuwa zikipitia.

"Ninawalaumu pakubwa baadhi ya wakazi wanaoendelea kujenga majumba kando ya barabara zinazopita nyuma ya soko hilo. Hatahivyo, masaroveya tayari wamepima barabara hiyo ili kubaini inakopitia na kabla ya mwisho wa wiki hii, ukarabati wa barabara hiyo utakuwa umeanza,” alisema Masira.