Wafanyabiashara wa kituo cha kibiashara cha Katito katika Kaunti ya Kisumu wamelalamikia usambazaji wa pesa bandia katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mmoja wa wafanyibiashara hao ambaye majuzi alilaghaiwa na wahuni hao waliomuibia kwa njia ya kununua bidhaa kwenye duka lake wakitumia noti bandia ya elfu moja, alitaka serikali kufanya upelelezi na kuwanasa wanaoendeleza kazi hiyo haramu.

Millcent Nyaugana anayemiliki duka la rejareja katika soko hilo aliwaambia Waandishi wa habari siku ya Jumatatu kuwa kuna baadhi ya watu wanaoshukiwa kusambaza pesa hizo kupitia kwa vijana wadogo na wanataka kujitajirisha kwa njia ya haraka bila kutoa jasho.

''Hawa ni watu ambao tunaweza kuwatambua iwapo maafisa wa upelelezi wataanza kulishughulikia swala hilo,'' alisema Nyaugana.

Gilbert Oriare anayeuza nafaka kwenye soko hilo ni mmoja wa wafanyibiashara hao anayekadiria hasara ya kiasi cha Sh25,000 baada ya kubadilishiwa noti kadhaa bandia kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita.

"Sana sana watu hawa huwa wanatulenga masaa ya jioni na wakati tunaposongwa na wateja,'' alisema Oriare.

Unapozuru kwenye maduka yaliyoko soko hilo, macho yako yatakuwa na mvuto kutazama picha za noti bandia zilizoanikwa ukutani baada ya wenye duka hizo kulaghaiwa na wahuni hao.