Wafanyibiashara katika soko la Kegogi wameitaka Kaunti ya Kisii kupitia idara ya kukusanyaji ushuru kuwajengea soko maalumu ili waweze kutekeleza biashara kwa njia ya kisasa.
Akiongea na Mwandishi huyu mnamo siku ya Jumatatu katika soko hilo la Kegogi, Mwenyekiti wa kundi cha wafanyibiashara hao kwa jina Vision Business Sacco Patrick Omariba alitaka mikakati kabambe kuwekwa itakayosaidia ujenzi wa soko hilo ili kuanzishwa haraka jinsi ilivyokuwa imependekezwa hapo mbeleni.
Wengi wa wafanyibiashara hao walipendekeza kuwa pesa zile zinazokusanywa ka ushuru kutumiwa katika upanuzi na ujenzi wa soko hilo ili kuboresha mazingira ya kufurahisha, hasa katika maeneo ya biashara.
“Kuna baadhi ya soko ambazo zilianzishwa nyuma ya soko hili letu na zimeendelea kuinuka zaidi baada ya kujengwa soko maalumu ambapo wafanyibiashara wanajivunia mauzo bora kwa kumiminikiwa na bidhaa aina nyingi zinazofikishwa sokoni na wafanyibiashara kutoka maeneo ya mbali kinyume na kama ilivyo katika soko hili letu,” alihoji Omariba.
Wafanyibiashara hao walikiri kuwa soko hilo linastahili kuwa na maendeleo ya kisasa ambapo ujenzi wa majumba ya biashara na makazi ya wafanyibiashara yanastahili kuwekwa kwenye miundo ya kisasa kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mengine kuwekeza kama njia mojawapo ya kuinua uchumi katika sehemu hiyo.
“Wawekezaji wakija hapa uchumi na biashara zetu zitaimarika vilivyo, lakini kwanza tunaomba tujengewe soko la kisasa,” alisema Beatrice Monari, mfanyibiashara katika soko la Kegogi.