Wafanyibiashara kutoka Keroka wamekosoa serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa kile walichokitaja kama kujikokota kuimarisha hali ya mazingira katika eneo hilo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa muungano wa wafanyibiashara katika eneo la Borabu Elkana Oremo, wafanyibiashara hao waliishtumu serikali ya kaunti kwa kujikokota kuimarisha hali ya mazingira hasa mabomba ya maji taka.
Wafanyibiashara hao aidha walilalamikia ukosefu wa maji yakutosha katika eneo hilo hata baada ya kaunti hiyo ndogo kuungoza katika ukusanyaji ushuru.
"Keroka ni mojawapo ya miji inayo ongoza kwenye ukusanyaji ushuru huku Nyamira. Ushuru ambao unafadhili miradi muhimu kwenye kaunti na tunashangazwa ni kwa nini pesa hizo hazitunufaishi hata kwa kutuletea maji ya mifereji," alisema Oremo.
Oremo aidha alitishia kuwaongoza wafanyibiashara wenzake kufanya maandamano dhidi ya serikali ya kaunti hiyo kulalamikia kutopokea huduma muhimu kutoka kwa usimamizi wa kaunti.
"Serikali ya kaunti haina budi ila kutufanyia kazi yakutupa huduma za maji safi ya kunywa na kutuhakikishia mazingira safi. Iwapo hayo hayataafikiwa, tutafanya maandamano na pia kuacha kulipa ushuru kwa serikali ya kaunti," alisema Oremo.