Wafanyibiashara katika soko kuu la Kongowea, Kaunti ya Mombasa, wameitaka, serikali ya kaunti kuwakarabatia miundomsingi ya soko hilo ili kupunguza maafa ambayo huenda yakachangiwa na mvua ya El Nino.
Wafanyibiashara hao walisema kuwa mabomba ya kupitisha maji, barabara za kuingia katika soko hilo pamoja na mabanda ya kuuzia bidhaa zao yako katika hali mbaya, na iwapo mvua ya El Nino itanyesha kwa wingi, huenda wakapata hasara kubwa mno kwa kupoteza mali yao huku wengi wao wakihifadhi bidhaa zao katika majumba yaliyo karibu na soko hilo.
Wakiongozwa na Benard Mutua ambaye ni katibu wa wauza mboga na matunda katika soko hilo siku ya Jumatatu, walidai kuwa bado serikali ya kaunti haijajiandaa vilivyo.
Walisema itakuwa vizuri serikali ya kaunti ya Mombasa kuanza kukarabati miundo msingi katika soko hilo mapema kabla ya kuanza kushuhudiwa mvua nyingi ambayo tayari walisema imeanza kuonyesha dalili.
“Kumekuwa na majanga ya mara kwa mara mvua inaponyesha kwenye eneo la pwani kwa jumla na wafanyabiashara wa soko hilo wamejipata katika hali ya kupoteza bidhaa zao kwa kusombwa na na maji ya mvua,” alisema Mutua.
Aliongeza kuwa hali ya soko hilo si ya kuridhisha na kumtaka Gavana wa kauti hiyo Hassan Joho, kuzingatia onyo ambalo lishatolewa na idara ya hali ya anga.
“Serikali ya kaunti inahitaji kuwajibika mapema na si lazima kungoja hadi janga au maafa kutokea ndio wachukue hatua. Mikakati sharti iwekwe mapema, kwani hili soko letu huenda likawa na shida kubwa zaidi, hivyo gavana wetu sharti ashughulike,” alisema Mutua.