Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyibiashara katika soko la Daraja Mbili iliyoko mjini Kisii wameiomba serikali ya kaunti hiyo kuweka vikingi katika barabara inayopita katikati mwa soko hilo ili kuzuia visa vya ajali vya kila mara.

Hii ni baada ya gari kupoteza mwelekeo hii leo, Jumatatu na kumgonga mfanyibiashara wa vitunguu aliyekuwa akiuzia kando kando mwa barabara hiyo inayotoka mjini Kisii kuelekea eneo la Suneka.

Visa vya aina hiyo vimekuwa vikishuhudiwa kila wakati katika soko hilo, haswa siku rasmi za soko, ikiwa Jumatatu na Alhamisi kila wiki.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wafanyibiashara hao, wakiongozwa na Martha Gesare waliomba serikali hiyo ya Kisii kujali maisha na maslahi yao na kuwawekea vikingi kwa soko hilo.

“Tunaomba madereva wanaohusiki na ajali kama hizi washikwe na kushtakiwa. Wengi wa madereva hao mara nyingi hutoroka baada ya kugonga mwanabishara na wanastahili kuendesha gari zao polepole wanapofika kwa soko hili,” alisema Kwamboka, mwanabiashara mwingine.

Aidha, wameomba serikali kuweka maafisa wa trafiki katika soko hilo, ili wawe wanaweka vizuizi na kuwashika wale wanaendesha magari kwa kasi wanapofika kwa soko hilo.