Wafanyibiashara katika eneo la Tudor wanahofia kukadiria hasara baada ya Chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa kufungwa kwa muda usiojulikana.
Wakizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, wafanyibiashara hao walisema kuwa wanahofia kuwa hatua hiyo ya kufungwa kwa chuo hicho itawaathiri pakubwa ikizingatiwa wateja wao wengi ni wanafunzi wa chuo hicho.
Mmoja wa wafanyibiashara hao, Susan Njeri, anaye uza chakula alisema huenda biashara yake ishuke kutokana kwa kukosekana kwa wateja wake.
“Toka wanafunzi waandamane na chuo hiki kufungwa, tayari biashara yangu imeanza kurudi chini,” alisema Njeri.
Kwa upande wake John Kimani, mmiliki wa 'cyber', alisema tayari ameanza kukosa wateja na ana hofia kuifunga biashara hiyo iwapo chuo hicho kitazidi kufungwa.
Wanafunzi wa Chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa waliandamana siku ya Jumatatu wakilalamikia kuongezwa kwa karo na hatimaye kuchoma magari mawili ya serikali ya kaunti ya Mombasa, jambo lililopelekea chuo hicho kufungwa.