Wafanyibiashara wa soko ya Magenche iliyoko eneo bunge la Bomachoge Borabu kaunti ya Kisii wamelalamikia uongonzi mbaya wa soko hilo na kuomba serikali ya kaunti ya Kisii kuingilia kati kutafuta suluhu.
Wakizungumza na mwandishi huyu wa habari siku ya Ijumaa katika soko hilo wafanyibiashara hao walikosoa kamati iliyochaguliwa mwaka wa 1999 kusimamia soko hilo kwa kusema kuwa kamati hilo lina uongozi mbaya.
"Tuaomba serikali itubadilishie kamati ambayo inasimamia soko hili. Kamati ambayo ilichaguliwa mwaka wa 1999 ndio inatumika hadi sasa na tunataka iondolewe,” alisema Maryrose Nyachama, muuzaji wa nguo.
Wakati huo huo, wafanyibiashara hao walisema kuna baadhi ya vyoo vilichimbwa katika soko hilo na havijawai kujengwa ili vianze kutumika.
Walisema kuwa shimo moja lilichimbwa mwaka wa 2005 na hadi sasa halijajengwa jambo ambalo limewalazimu kuomba serikali kulitatua.
“Choo kikichimbwa bila kujengwa ni ishara ya kuonyesha uongonzi mbaya ulioko katika soko hili. Tangu mwaka wa 1999 ni Rais wangapi wameng’atuka mamlakani? Daniel Moi alikuwa wakati huo, pia Mwai Kibaki amenga’tuka uongonzini mbona hawa wanakamati wa soko hili nao wazingatuke?” auliza Peter Misati, mfanyibiashara.
Wafanyibishara hao wameapa kusimama kidete mpaka wakati serikali itakapoingilia kati na kuchagua kamati ingine tofauti itakayosimamia uongonzi wa soko hilo.
Waliwaomba machifu wa eneo hilo kuingilia kati ili kuokoa wafanyibiashara wa soko hilo.