Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyikazi zaidi ya 100 walioajiriwa katika Bunge la Kaunti ya Kisii kwa miezi 10 iliyopita waliandamana hadi ofisi ya Spika wa bunge la kaunti yhiyo Okerosi Ondieki ili kuambiwa kwa nini hawajalipwa mshahara tangu waajiriwe.

Wafanyikazi hao wakiongozwa na Vincent Onyango, waliandamana siku ya Jumatano katika mji wa Kisii kuelekea ofisi ya spika kuelezwa kwa nini hawajalipwa mshahara wao huku wakidai bajeti iliyosomwa katika bunge la kaunti hiyo siku ya Jumanne ilisema kuna pesa zilirudishwa kwa serikali kuu, na serikali hiyo inasema kuwa hawajawahi lipwa kwa ukosefu wa pesa.

"Zile pesa ambazo zilirudishwa kwa serikali kuu zilitoka wapi, kama za kulipwa wafanyikazi kama sisi hamna?. Tumekuwa tukiishi kwa madeni tangu tuajiriwe na serikali ya Kaunti ya Kisii na tumepata aibu kubwa mahala tunatoka ndio maana tunahitaji kuambiwa kwa nini hatulipwi pesa zetu,” alisema Onyango, mmoja wa wafanyikazi hao.

Wafanyikazi hao waliweka kambi nje ya makao ya Bunge ya Kaunti ya Kisii, jambo ambalo liliwalazimu Wawakilishi wawili wa Wadi ya Boochi Shem Ondara na wa Wadi ya Baasi Henry Moracha ambaye pia ni kiongonzi wa walio wengi kuingilia kati na kuomba wafanyikazi hao walipwe kwani wamekuwa wakifanya kazi tangu waajiriwe.

Wafanyikazi hao waliajiriwa mwezi Septemba tarehe 3 mwaka jana na hawajalipwa kwa madai kuwa waliajiriwa kwa njia isiyo halali kupitia spika wa bunge hilo Ondieki ambaye hakuwa katika ofisini mwake hiyo jana walipoandamana kwani alikuwa ameenda kuhudhuria mkutano mahala pengine ambapo hangeweza kuwazungumzia.

Baadhi ya waandamanaji hao walisema spika huyo aliwaambia kuwa wapime sare za kufanya kazi hapo mbeleni ili wawe safi na wakafanya hivyo huku wengine wakisema walikopa pesa ya kununua nguo hizo wakiongeza kuwa wengine walikopa kutoka kwa benki na imekuwa vigumu kurudisha hizo pesa maana hawajalipwa kwa wakati huo wote.

Wawakilishi hao (Ondara na Morancha) waliiomba tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) kuingilia kati kuchunguza suala hilo.