Wafugaji wa mifugo katika eneo la Kikuyu wameonywa dhidi ya kutembeza mifugo wao barabarani kwa kuwa wanasababisha msongamano wa magari na pia ajali.
Hii ni baada ya mfugaji mmoja kutiwa mbaroni baada ya kutembeza mifugo wake zaidi ya hamsini barabarani kisha kusababisha msongamano mkubwa katika barabara ya Southern bypass.
Akidhibitisha kisa hiki siku ya Ijumaa, Komanda wa trafiki katika eneo la Kikuyu, Inspekta Elizabeth Wakuloba alisema kwamba wafugaji wenye tabia hiyo wanakiuka sheria za barabarani.
Alisema kwamba wafugaji hukiuka sheria na wanapokamatwa hulamika kwamba hawana barabara nyingine.
Hata hivyo, Inspekta Wakuloba alisema kwamba ni hatia kwa wafugaji kufanya hivyo kwa kuwa wanahatarisha mifugo yao na pia maisha ya wanaotumia barabara.
Inspekta alieleza kwamba atakaye patikana atashtakiwa.
"Naonya wafugaji mifugo dhidi ya kutembeza mifugo wao barabarani kwa kuwa ni hatia.Mifugo hao hawajui sheria na watakapo patikana, mfugaji atakamatwa na kushtakiwa," alisema Wakuloba.
Aliwashauri wafugaji kuwafuga mifugo wao nyumbani na kuwataftia chakula badala ya kuwatoa nyumbani na kuvunja sheria za barabarani ambazo zitawatia mashakani.