Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wenye mifugo katika kaunti ya Kisii wametahadharishwa dhidi ya kuzuka kwa maradhi mabaya ya mifugo katika msimu huu unaotarajiwa wa El Nino, na kutakiwa kuwa macho na tayari kuwapa wanyama wao dawa za kuzuia maradhi hayo.

Akiongea siku ya Alhamisi kwenye hafla iliyowakutanisha washikadau katika harakati za kukabili tatizo hilo la mvua ya El Nino katika ukumbi wa taasisi ya mafunzo ya wakulima iliyoko katika mji wa Kisii, mkurugenzi wa mifugo katika kaunti ya Kisii, John Ndege alisema kuwa mifugo wataathirika zaidi na sharti wakazi wajiandae kwa kuhakikisha kuwa wanyama wao wanapewa chakula pamoja na maji safi.

Ndege alisisitiza kuwa wakulima pamoja na wafugaji watafute ushauri kutoka kwa maafisa wa mifugo katika maeneo wanamokaa, na washiriki katika mikutano ambayo itakuwa ikiandaliwa na idara hiyo na idara nyingine za serikali kwa kuwapa wakazi taarifa kuhusiana na athari za mvua hiyo.

Aliwashauri maafisa wa mifugo katika wilaya, kata, pamoja na lokesheni kuhakikisha kuwa ujumbe unawafikia wakazi hasa jinsi ya kuwaangalia mifugo wao ili wasije wakaathiriwa.

“Wafugaji wawe makini katika msimu huu, na sharti wachunge mifuga yao dhidi ya maradhi kwa kuwapa maji safi na nyasi ambayo ni nzuri ili kuzuia kusambaa kwa maradhi kupitia maji au nyasi,” alisema mkurugenzi huyo.

Akiongea katika mkutanao huo, afisa mkuu katika wizara ya kilimo katika kaunti ya Kisii alitoa wito kwa kila afisa ambaye alishiriki kwenye mkutano huo kuhakikisha kuwa atawajibikia kazi yake ambayo ni kuandaa mikutano kila wiki mara mbili ili kuwaelimisha wakazi kwenye sekta zote ambazo huenda zikaathiriwa na mvua hiyo ya Elnino.