Waganga mjini Mombasa wamejitokeza na kukashfu hatua ya maafisa tawala pamoja na maaskari wa kaunti ya Mombasa kwa kuyang’oa mabango ya kutangaza biashara zao za kuwavutia wateja wao.
Kulingana na waganga hao, hatua ya kutundika kwa mabango hayo ya kutangaza biashara zao kamwe hayahusiki kivyovyote na uharibifu wa mazingira ya mji wa Mombasa, na wakaitaka serikali kuu na kaunti ya Mombasa kukoma kuwaingilia na kazi zao.
Wakizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, baadhi ya waganga hao wakiongozwa na Kadzigwe Nyae Wanga walisema kwamba hawajaridhishwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa serikali kuu na wale wa kaunti ya Mombasa kuwadhalilisha na kazi zao.
"Hatujaridhiswa na hatua ya serikali kutuvunjia mabango yetu na kutudhalilisha mbele ya umma kwamba kazi tunayofanya sio halali, na wengine wakituita sisi wachawi hilo sisi kama waganga halali hapa Mombasa hatutakubaliana nalo kamwe, na ikiwezekana tutashtaki wale tutakaowaona wakituita sisi ni wachawi," alisema Nyae.
Aidha, wamewataka wakazi pamoja na wadau wanaoshinikiza kung’olewa kwa mabango hayo kuheshimu kazi zao, kwani ndio biashara wanazotegemea kujipatia riziki, huku wakisema kwamba wana vibali halali vya kuendesha biashara hiyo ya uganga nchini.
Kauli ya waganga hao imejiri baada ya Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kuagiza kung’olewa kwa mabango ya waganga katikati mwa mji wa Mombasa kutokana na 'kuharibu mazingira' ya mji, huku akishikilia kwamba mji wa Mombasa ni kivutio kikuu kwa watalii.
Waganga mjini Mombasa wamesema kwamba hawajaridhiwa na hatua ya serikali kuu na ile ya kaunti ya Mombasa kuwadhalilisha na kusema kwamba hao sio waganga halali.