Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi wamewatia mbaroni wagema 15 kutoka Lokesheni ya Taraacha eneo bunge la Nyaribari Chache, baada ya kufumaniwa wakiendelea kutengeneza pombe haramu ambayo ni kinyume na sheria.

Maafisa hao wa kituo cha Kisii wakiongozwa na chifu wa lokesheni hiyo Kennedy Atemba, walifanya msako huo siku ya Jumatatu.

Haya yanajiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa pombe haramu haikubaliwi kuuzwa nchini jambo ambalo baadhi ya wagema hawajaliitikia kikamilifu.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika eneo hilo la Taraaja, Chifu Atemba alisema waliotiwa mbaroni watafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kukiuka sheria kwa kuendelea kutengeneza na kuuza pombe haramu.

“Hawa wagema ambao wametiwa mbaroni watakabiliwa kisheria kwani utengenezaji wa pombe haramu ulifutiliwa mbali lakini wengine hawataki kuitikia wito wa serikali na watakabiliwa vilivyo,” alisema Atemba.

Aliongezea, “Naomba wale ambao wanaendelea kutengeneza pombe wasitishe biashara hiyo kabla hatujawafikia kwani ni kunyume na sheria kuendelea kutengeneza pombe haramu nchini.”